Wednesday 2 January 2008

YA KWELI HAYA? AMUA MWENYEWE

Sijui kama habari hizi ni kweli, lakini kama ni kweli Watanzania tuna hali mbaya.

Yasemekena kuwa kwenye kikao cha Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kilichochagua uongozi mpya kilichomalizika Dodoma hivi karibuni Waziri Mkuu Edward Lowassa, na Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba hawakupata zile kura ambazo zilitangazwa na vyombo vya habari baada ya uchaguzi.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi kwa vyombo vya habari, katika kundi la wagombea 20 kura za Lowassa zilikuwa 1,681, akifuatiwa na Andrew Chenge (1,530), na Yusuph Makamba (1,510).

Kwa mujibu wa habari hizo hizo, wengine walioshinda kwenye kundi hilo ni Bernard Membe (1,281), Jaka Mwambi (1,239), Profesa Juma Kapuya (1,216), Abdulrahman Kinana (1,204), Christopher Gachuma (1,181), Aggrey Mwanri (1,068), Stephen Wassira (1,107), Makongoro Mahanga (1,067), Frederick Sumaye (1,065), John Komba (1,056), Kingunge Ngombale Miwiru (1,023), William Lukuvi (943), John Chiligati (910), Amos Makala (871), Profesa Samwel Wangwe (817), Profesa David Mwakyusa (754), na Jackson Msome (747).

Habari zisizo rasmi zinasema kuwa uwkeli ni kuwa Lowassa na Makamba hawakupata kura za kutosha kushinda nafasi zao na kulichotokea ni kuwa waliondolewa wagombea wawili waliyoshika nafasi ya 19 na 20 ili kutoa nafasi kwa washindwa hao. Aidha, ili kuwapa hadhi inayofanana na nyadhifa zao, walipachikwa ushindi wa namba moja (Lowassa), na namba tatu (Makamba).

Habari zisizo rasmi zinaendelea kusema kuwa aliyeshika nafasi ya kwanza kwenye kundi la 20 alikuwa Andrew Chenge, na ya pili ilichukuliwa na Christopher Gachuma.

Hali mbaya kwa Watanzania inakuja kwa namna mbili. Kwanza, kama haya ni ya kweli ina maana Waziri Mkuu Lowassa na Katibu Mkuu Makamba hawaungwi mkono na chama chao wenyewe kwa sababu ambazo ingekuwa vizuri kwa Watanzania kuzifahamu. Na kama Lowassa hakubaliki kwenye chama chake, Watanzania wengine tuna sababu gani ya kumkubali? Katibu Mkuu wa CCM ni wa wana CCM pekee, lakini Waziri Mkuu anaongoza Watanzania wote, wenye vyama na wasiyo na vyama, hivyo ni haki ya kila Mtanzania kufahamu kwa nini Lowassa hakupata kura za kutosha kushika nafasi muhimu katika uongozi wa juu wa chama chake?

Pili, kama Andrew Chenge ndiyo kweli aliongoza kundi la 20, na Christopher Gachuma alikuwa wa pili, na baadae taarifa zinatueleza kuwa Chenge kashika nafasi ya pili, na Gachuma kashika nafasi ya saba tuna uhakika gani na ukweli wa hayo majina mengine kwenye orodha hiyo na kura zao? Tunaweza kuuliza: tuna hakika gani na matokeo yote ya uchaguzi huo muhimu kwa CCM na kwa Tanzania?

NA MENGINE HAYA, SIJU NAYO KWELI?

Inasemekana kuwa Waziri Mkuu Lowassa ananuwia kugombea urais 2010. Ndiyo, 2010, siyo 2015 kama ambavyo imekuwa desturi ya CCM kumuacha rais aliye madarakani kuongoza kwa vipindi viwili vya miaka mitano.

Sasa hizi zinaweza kuwa ni porojo tu za washindani wenzake wanaowania urais mwaka 2015. Lakini kuna muelekeo kuwa atawania urais mwaka 2015.

Matarajio ni kuwa atakapochukuwa fomu kuwania urais mwaka 2015 hawa CCM wenzake waliyombwaga chini Dodoma hivi karibuni hawatakuwepo kwenye Mkutano Mkuu utakaochagua mgombea urais wa CCM, na kama wakiwepo basi Watanzania tutatarajia kuwa watambwaga tena chini, au wakimpitisha watueleze imekuwaje mwaka 2007 alikuwa hafai, na mwaka 2015 mpaka 2025 anafaa?

Kama haya yote ni kweli, siku Edward Lowassa anaapishwa kuwa Rais wa Tanzania kwa kipindi cha 2015 mpaka 2025 Watanzania itabidi tucheke sana. Tena sana tu. Au sijui itabidi tulie?

Somo la leo: Tumewachagua sisi wenyewe, wewe na mimi

Foti Mwarobaini