Saturday 3 January 2009

Angekuwepo Juliasi…

Ni dhahiri kuwa Mwalimu Nyerere angekuwa yuko Tanzania leo hii, kiwango cha tuhuma za ufisadi tunachokiona Tanzania hivi leo kisingeonekana. Kwa sababu hakuwa kiongozi wa kunyamazia viongozi wanaovunja maadili na dhamana wanayopewa na wananchi.

Kwamba kiongozi haoni aibu kukiri kuwa ana 'vijisenti' vipatavyo dola milioni moja kwenye akaunti yake binafsi ni kielelezo cha nyakati zetu za sasa. Haya yasingeweza kutokea kwenye serikali ya awamu ya kwanza, na yasingeweza kutokea kwenye Serikali hii kama Nyerere angekuwepo.

Pamoja na porojo tunazoambiwa na viongozi wetu kuhusu nia yao kubwa ya kumuenzi Nyerere, ukweli ni kuwa hawafanyi hivyo. Na pengine ni kweli kuwa wanajuta kuzaliwa kwenye nchi moja na Nyerere. Kwa sababu ndiye tunayemtumia kuwapima viongozi waliyomfuata. Na ndiyo hayo yanayowafanya Watanzania wengi kuona kuwa tuhuma za sasa dhidi ya viongozi wetu zinavunja imani ya wananchi juu ya viongozi wao, na zinahatarisha amani ambayo tunaambiana bado iko Tanzania.

Na siyo yeye tu, tunawapima pia kwa kuwalinganisha na viongozi wengine kama Mwinyi, Sokoine, Kawawa, Msuya, Warioba, na wengine. Sina maana kuwa hawa wote wana sifa zinazofanana. Hoja ni kuwa kitu au mtu hawezi kuwa mbaya au mzuri bila kulinganishwa na mtu mwingine.

Miaka 100 kutoka leo Watanzania watashindwa kutofautisha kati ya aina ya viongozi wenye vijisenti kwenye visiwa vya ughaibuni, na wananchi ambao hawakuchukuwa hatua yoyote ile kurudisha uadilifu kwenye uongozi wa nchi yao ili kuondokana kabisa na viongozi wa aina hiyo.

Au labda hili nalo linahitaji wafadhili?