Sunday 9 November 2008

Serikali inatuangusha

Kuna habari zilitangazwa Mei 2008 kuwa Serikali ya Tanzania itachukuwa hatua za kisheria dhidi ya kampuni ya Norconsult kwa tuhuma kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuendesha biashara bila kuandikishwa, na kukwepa kulipa kodi.
 
            Habari kamili :
            http://allafrica.com/stories/200805090429.html
 
Kuna msemo wa Waingereza: Closing the stable door after the horse has bolted. Una maana kitendo cha kuchukuwa hatua baada ya athari kutokea.
 
Norconsult imefanya kazi Tanzania bila kuandikishwa kwa miaka kumi bila bugudha. Inakisiwa kukwepa kodi zipatazo Sh.2.4 bilioni. Imeshinda kandarasi kusimamia miradi mikubwa ya ujenzi ikiwa ni pamoja na barabara ya Sengerema - Busagara (Sh.35.7 bilioni), na barabara ya Marangu - Rombo Mkuu (Sh.23.3 bilioni).
 
Haiingii kichwani kuwa kampuni imepata kazi kubwa kama hizo Serikalini na hamna mamlaka yoyote iligunduwa kuwa kuna walakini. Kwa miaka kumi!
 
Hapa kinachoonekana kutokea ni makundi yenye maslahi ya kisiasa na uchumi yameanza kupambana kwa kutoleana siri zao. Na hii inatokea sana kwenye mifumo ya siasa ambapo kundi moja likishinda uchaguzi hutokea kujaribu kuhodhi madaraka yote ya kisiasa, kiuchumi, na kijamii na kusababisha kundi lililonyimwa fursa linapoingia madarakani kulipiza kisasi.
 
Kuna msemo wa Kiswahili: Vita vya panzi ni furaha ya kunguru. Msemo unaofaa katika mazingira haya ni: Kunguru (wakubwa) wakigombana, panzi (raia) wanapata ahueni.

Friday 31 October 2008

Nchi Inakwenda Kombo

Pamoja na kwamba Serikali inasema mambo yanakwenda vizuri, ukweli ni kuwa Serikali inaelemewa na matatizo ya kila aina.

Migomo ya walimu, ya wanafunzi, ya wafanyakazi. Kushindwa kwenye uchaguzi mdogo wa jimbo la Tarime, na hivi karibuni wastaafu wa Shrika la Bandari kuvua nguo barabarani wakishinikiza Serikali kulipwa mafao yao.

Serikali ikiendelea kujidanganya kuwa hakuna tatizo, itaendelea kupoteza majimbo ya uchaguzi kwenye Uchaguzi Mkuu 2010.

Wednesday 29 October 2008

Kimya Kikubwa Kina Mshindo

Nimekuwa kimya kwa muda, lakini nitaanza tena kuandika kwenye blog hii baada ya muda si mrefu.

Yako mengi ya kusema, lakini nitachagua yale muhimu katika kuchangia mawazo mbalimbali.

Saturday 10 May 2008

Robert Gabriel Mugabe

Hawapo wengine watakofuata nyayo za kina Mugabe.

Ni kweli, Mugabe amechelewa kuchukuwa hatua zilizoifikisha Zimbabwe hapo ilipo lakini ukweli ni kuwa kosa lake kubwa ni kupingana na Wamarekani na Waingereza, na suala zima la vikwazo vya uchumi dhidi ya Zimbabwe kwa sababu ku kutokubali kwake kuimba ngonjera zinazotungwa Washington na London.

Viongozi wa kizazi kipya, wakina Tsvangirai, haiwasumbuwi kuweka maslahi ya nchi pembeni kwa kisingizio cha

Saturday 26 April 2008

Wanaanza kuanguka, mmoja baada ya mwingine.

Alianza Edward Lowassa, akafuata Ibrahim Msabaha, na muda haukupita, Nazir Karamagi akaaachia ngazi.

Kwa kasi hii, tunaweza kufika mwaka 2010 ikawa hatuna kiongozi hata mmoja ambaye hajaguswa na Kiwanda cha Kashfa cha Tanzania (KKT).

Niliwahi kutabiri, bila kuwa na ushahidi madhubuti, kuwa itakapofika 2015 Tanzania itakuwa na nafasi ya kupata Rais safi, ambaye hana kashfa wala marafiki wenye kashfa, na ambaye hataogopa kuchukuwa hatua dhidi ya wale wenye tuhuma za kashfa.

Wednesday 2 January 2008

YA KWELI HAYA? AMUA MWENYEWE

Sijui kama habari hizi ni kweli, lakini kama ni kweli Watanzania tuna hali mbaya.

Yasemekena kuwa kwenye kikao cha Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kilichochagua uongozi mpya kilichomalizika Dodoma hivi karibuni Waziri Mkuu Edward Lowassa, na Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba hawakupata zile kura ambazo zilitangazwa na vyombo vya habari baada ya uchaguzi.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi kwa vyombo vya habari, katika kundi la wagombea 20 kura za Lowassa zilikuwa 1,681, akifuatiwa na Andrew Chenge (1,530), na Yusuph Makamba (1,510).

Kwa mujibu wa habari hizo hizo, wengine walioshinda kwenye kundi hilo ni Bernard Membe (1,281), Jaka Mwambi (1,239), Profesa Juma Kapuya (1,216), Abdulrahman Kinana (1,204), Christopher Gachuma (1,181), Aggrey Mwanri (1,068), Stephen Wassira (1,107), Makongoro Mahanga (1,067), Frederick Sumaye (1,065), John Komba (1,056), Kingunge Ngombale Miwiru (1,023), William Lukuvi (943), John Chiligati (910), Amos Makala (871), Profesa Samwel Wangwe (817), Profesa David Mwakyusa (754), na Jackson Msome (747).

Habari zisizo rasmi zinasema kuwa uwkeli ni kuwa Lowassa na Makamba hawakupata kura za kutosha kushinda nafasi zao na kulichotokea ni kuwa waliondolewa wagombea wawili waliyoshika nafasi ya 19 na 20 ili kutoa nafasi kwa washindwa hao. Aidha, ili kuwapa hadhi inayofanana na nyadhifa zao, walipachikwa ushindi wa namba moja (Lowassa), na namba tatu (Makamba).

Habari zisizo rasmi zinaendelea kusema kuwa aliyeshika nafasi ya kwanza kwenye kundi la 20 alikuwa Andrew Chenge, na ya pili ilichukuliwa na Christopher Gachuma.

Hali mbaya kwa Watanzania inakuja kwa namna mbili. Kwanza, kama haya ni ya kweli ina maana Waziri Mkuu Lowassa na Katibu Mkuu Makamba hawaungwi mkono na chama chao wenyewe kwa sababu ambazo ingekuwa vizuri kwa Watanzania kuzifahamu. Na kama Lowassa hakubaliki kwenye chama chake, Watanzania wengine tuna sababu gani ya kumkubali? Katibu Mkuu wa CCM ni wa wana CCM pekee, lakini Waziri Mkuu anaongoza Watanzania wote, wenye vyama na wasiyo na vyama, hivyo ni haki ya kila Mtanzania kufahamu kwa nini Lowassa hakupata kura za kutosha kushika nafasi muhimu katika uongozi wa juu wa chama chake?

Pili, kama Andrew Chenge ndiyo kweli aliongoza kundi la 20, na Christopher Gachuma alikuwa wa pili, na baadae taarifa zinatueleza kuwa Chenge kashika nafasi ya pili, na Gachuma kashika nafasi ya saba tuna uhakika gani na ukweli wa hayo majina mengine kwenye orodha hiyo na kura zao? Tunaweza kuuliza: tuna hakika gani na matokeo yote ya uchaguzi huo muhimu kwa CCM na kwa Tanzania?

NA MENGINE HAYA, SIJU NAYO KWELI?

Inasemekana kuwa Waziri Mkuu Lowassa ananuwia kugombea urais 2010. Ndiyo, 2010, siyo 2015 kama ambavyo imekuwa desturi ya CCM kumuacha rais aliye madarakani kuongoza kwa vipindi viwili vya miaka mitano.

Sasa hizi zinaweza kuwa ni porojo tu za washindani wenzake wanaowania urais mwaka 2015. Lakini kuna muelekeo kuwa atawania urais mwaka 2015.

Matarajio ni kuwa atakapochukuwa fomu kuwania urais mwaka 2015 hawa CCM wenzake waliyombwaga chini Dodoma hivi karibuni hawatakuwepo kwenye Mkutano Mkuu utakaochagua mgombea urais wa CCM, na kama wakiwepo basi Watanzania tutatarajia kuwa watambwaga tena chini, au wakimpitisha watueleze imekuwaje mwaka 2007 alikuwa hafai, na mwaka 2015 mpaka 2025 anafaa?

Kama haya yote ni kweli, siku Edward Lowassa anaapishwa kuwa Rais wa Tanzania kwa kipindi cha 2015 mpaka 2025 Watanzania itabidi tucheke sana. Tena sana tu. Au sijui itabidi tulie?

Somo la leo: Tumewachagua sisi wenyewe, wewe na mimi

Foti Mwarobaini