Tuesday 3 February 2009

Wizi Mtupu

Matukio nchini Tanzania ya miaka ya hivi karibuni ni matunda ya jitihada kubwa ambazo zimefanywa na kundi dogo la Watanzania miaka iliyopita kuhujumu rasilimali za Taifa kwa kiwango cha hali ya juu kabisa. Kwa msemo mwingine, kwa kiwancgo cha lami.

Leo kila kukicha, tunasoma habari kuhusu namna ambavyo Watanzania hawa, wengi wao ambao ama walikuwa viongozi wenye nyadhifa mbalimbali Serikalini, au ni watu waliyokuwa na uhusiano na voingozi Serikalini, walivyopanga mipango mbalimbali kuchota pesa za umma kwa manufaa yao binafsi.

Baba lao kati ya hizi njama inajulikana kama kashfa ya EPA ambayo inahusisha kundi la walaji kuchota pesa zilizokuwa kwenye akaunti maalum ya kulipa madeni nje ya nchi, pesa ambazo zilikuwa zikisubiri upatikanaji wa fedha za kigeni ili zitumwe kwa makampuni ya nje ambayo yalikuwa yameuzia kampuni au mashirika ya Tanzania bidhaa mbalimbali.

Wajanja wakaamua kukwapua hizo pesa na leo hii, polepole, zinaendelea kufichuka habari kuhusu wizi huo wa mabilioni ya pesa.

Jambo la kustaajabisha ni kuona jinsi gani hawa Watanzania walipata ujasiri wa kuendesha vitendo hivi kinyume na sheria bila woga kuwa siku za mwizi siyo bilioni moja, ni arobaini tu.

Chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM) hakina budi kuchukuwa hatua zaidi dhidi ya watuhumiwa siyo wa wa EPA tu lakini wa kashfa nyingine zote ambazo siyo tu zinatishia kuendelea kwa CCM kuongoza Serikali, hasa tukizingatia kuwa uchaguzi mkuu wa 2010 unakaribia, lakini kutochukuwa hatua madhubuti kunaweza kuhatarisha uhai wa nchi na hata usalama wake. Wananchi wanapokosa imani juu ya uwezo wa Serikali wa kutetea maslahi yao na ya nchi huwa wako tayari kuchukuwa hatua ambazo zinapingana na sheria.

Hivi karibuni shekhe mmoja wa Mwanza ametamka kuwa haina haja kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wa mauaji ya albino. Alisema wakamatwe, wafikishwe hadharani, na wapigwe risasi. Serikali ya CCM isipochukuwa hatua madhubuti kupunguza tsunami hii ya rushwa, mamneno ya huyo shekhe yataanza kuonekana halali kutumika dhidi ya watuhumiwa wa kashfa lukuki za rushwa ambazo zinaindama Tanzania.

Rais Kikwete alitamka mjini Tanga miaka michache iliyopita kwa utaratibu unaoruhusu viongozi kuwa na maslahi ya kibiashara umepunguza imani ya wananchi kwa viongozi na Serikali yao. Tatizo limeonekana, na dawa inajulikana. Labda mdunga sindano na mambomba ya sindano ndiyo vinakosekana.

No comments: